Halmashauri ya manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Plan International imeunda baraza la watoto la wilaya hiyo litakalokuwa na lengo la kutetea na kulinda haki za watoto.
Akizungumza katika kikao cha uundaji wa baraza hilo afisa maendeleo wa manispaa ya Ilemela ndugu Sitta Singibala amesema kuwa manispaa yake imekuwa na dhamira ya kuwakutanisha watoto katika chombo kimoja kujadili changamoto zinazowakabili na kushiriki namna ya kuzitatua jambo ambalo litafanikiwa kwa uwepo wa baraza la watoto wilayani humo sambamba na kushukuru shirika lisilo la kiserikali la Plan International lililokubali kushirikiana na manispaa yake kuunda baraza hilo.
‘.. Tumekuwa na dhamira ya kuwakutanisha watoto pamoja kupitia mabaraza yao kujadili changamoto zinazowakabili ili washiriki kuzipatia ufumbuzi, Tunawashukuru wenzetu wa plan kutusaidia katika kufanikisha uundaji wa baraza la watoto wilayani kwetu ...’ Alisema
Uundaji wa baraza hilo ulienda sambamba na zoezi la uchaguzi la kupata viongozi kwa nafasi mbalimbali za baraza hilo ambapo kwa nafasi ya mwenyekiti wa baraza la watoto wilayani humo alichaguliwa ndugu Aidath Ismail makamu mwenyekiti alichaguliwa ndugu Aisha Bakari, katibu alichaguliwa ndugu Neema Paul na mweka hazina alichaguliwa ndugu Alony Steven
Kwa upande wake muwakilishi wa taasisi ya Plan International ndugu Emmanuel Asaph mbali na kuelezea juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na asasi yake katika kusaidia watoto ameipongeza wilaya ya Ilemela kwa kuwa mstari wa mbele katika uundaji wa mabaraza hayo ukilinganisha na wilaya zingine za mkoa wa Mwanza ambazo hata mabaraza ya kata hayajaundwa.
Mratibu wa baraza la watoto wilaya ya Ilemela Bi Sara Nthangu amewataka viongozi waliochaguliwa kushirikiana na walezi wao katika kuandaa mpango kazi wa baraza hilo pamoja na kuwasilisha mada mbalimbali kwa watoto hao ikiwemo maana ya baraza hilo, sheria ya mtoto na haki zake, tafsiri ya mtoto, chimbuko la baraza, umuhimu wa baraza, wajibu wa watoto, wajibu wa serikali na wadau kwa baraza pamoja na majukumu ya viongozi wa mabaraza ya watoto.
Mkutano huo wa uundaji wa baraza la watoto wilaya ya Ilemela pia ulihudhuriwa na mwenyekiti wa baraza la watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Joel Festo Kiumbu, makamu mwenyekiti wa baraza hilo taifa ndugu Apyamwene Nicholaus, mwenyekiti wa baraza la watoto mkoa wa Mwanza ndugu Neema Theonest na watendaji wa kata na maafisa maendeleo wa manispaa kama walezi wa mabaraza hayo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.