Baraza la Madiwani la Manispaa ya Ilemela limejengewa uwezo juu ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA, mafunzo hayo yameendeshwa na wataalam wa Kitengo cha TEHAMA Ilemela
Waheshimiwa Madiwani hao wameshukuru kwa mafunzo hayo ambapo wameipongeza serikali kwa kuanzisha mfumo huu unaoenda kuipunguzia halmashauri gharama za uendeshaji wa vikao kuanzia kudurufu makabrasha hadi usambazaji wake.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe. Renatus Mulunga amesema kuwa, mfumo huu utakuwa na manufaa kwa sababu unaenda kupunguza gharama za kuandaa makrabasha, itaokoa muda wa kusambaza makabrasha, huku akiwataka Madiwani kuutumia mfumo huu kwa kadri ya maelekezo yatakayotolewa.
Akizitaja faida za mfumo huu Mhe. Sarah lisso amesema kuwa umerahisisha mawasiliano kwani kwa sasa unaweza kuhudhuria kikao popote pale ulipo kwani utatumiwa nyaraka na itaonyesha kama umekubaliana na umepokea nyaraka hizo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia kitengo cha TEHAMA imeendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA ambapo imefanikiwa kuanza kutumia mifumo wa E-BOARD na Mfumo wa Ofisi Mtandao, kwa ajili ya kuendesha shughuli za ofisi ikiwemo uendeshaji wa vikao pamoja na Shughuli zinazohusu mzunguko wa mafaili na nyaraka ndani na miongoni mwa taasisi za umma.
Isack Tanguye, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA amefafanua juu ya mifumo hii na kusema kuwa E- Board ni mfumo uliosanifiwa na serikali mtandao kwa ajili ya uendeshaji wa vikao mbalimbali vya halmashauri, ambao unaenda kupunguzia taasisi gharama za uendeshaji wa vikao, utasaidia kufuatilia yatokanayo ya vikao ikiwa ni pamoja na kufahamu agenda za vikao, ni mfumo rafiki
Ameongeza kusema kuwa Mfumo wa Ofisi Mtandao umetengenezwa ili kuwezesha na kurahisisha shughuli za utawala za kila siku ndani ya Serikali. Shughuli hizo zinahusu mzunguko wa mafaili na nyaraka ndani na miongoni mwa taasisi za umma.
Serikali imeboresha na inaendelea kuboresha miundombinu na mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao kwa umma kwa uwazi na kwa gharama nafuu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.