Baraza la madiwani limemuelekeza mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Wakili Kiomoni Kiburwa Kibamba kuhakikisha kuwa analipa fidia katika maeneo yote yaliyotwaliwa na manispaa hiyo kwa shughuli za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili yaweze kumilikiwa na umma.
Rai hiyo imetolewa na Mstahiki Meya Mhe Mulunga wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichoketi kwa ajili ya kujadili taarifa za utekelezaji katika kipindi cha robo ya pili yam waka wa fedha 2023/2024 (Oktoba hadi Disemba) ambapo amefafanua kuwa upo umuhimu mkubwa wa kutwaa maeneo kwa kulipa fidia na kuyalinda kwa ajili ya shughuli za umma kama ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na shule
“ Niwapongeze na kuwashukuru viongozi waliokuwepo wakati Hayati Mwalimu Nyerere anatangaza vijiji vya ujamaa ambapo maeneo kama ya Sangabuye wakachukua eneo kubwa sana, wasingechukua maeneo makubwa hata ile sekondari ya Sangabuye isingekuwepo, Mkurugenzi tumia maarifa yako yote, uwezo wako wote, sheria zako zote hakuna kuachia hata kipande cha ardhi tulichokitwaa.” Alisema Mhe Mulunga
Aidha Mhe Mulunga amewaasa viongozi kufikiria vizazi vijavyo pindi wanapopanga mipango ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo pamoja na kutanguliza maslahi ya umma badala ya kujifikiria wao binafsi ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na rasilimali za nchi zilizopo
Akichangia mjadala huo, Wakili Wilbard Kilenzi diwani wa kata ya Ilemela alishauri baraza la madiwani la kuhakikisha linasimamia msimamo wa kutorejesha maeneo yaliyotwaliwa kwa shughuli za umma kwa kuwa kufanya kinyume chake ni kuiingiza Manispaa hasara kwani itapaswa kulipa gharama zaidi za fidia kwa waliotwaliwa maeneo yao kutokana na kuwasitishia kuendeleza maeneo yao kwa muda mrefu na hivyo kusisitiza juu ya suala la ulipaji wa fidia kwa maeneo hayo yaliyotwaliwa.
Baadhi ya madiwani kwa nyakati tofauti walishauri kuwa ni vyema halmashauri ikaweka utaratibu wa kutenga fedha kila mwezi kwa ajili ya malipo ya fidia ili kuondokana na deni hili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela wakili Kiomoni Kibamba alifafanua hoja hiyo kwa kusema, kuwa zaidi ya shilingi bilioni 5.9 zinadaiwa na wananchi kwa ajili ya fidia kutokana na Serikali kutwaa maeneo yao kwa shughuli mbalimbali za maendeleo na kwamba Manispaa yake itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya fidia hizo na kusema kuwa kwa maeneo yote ambayo yameshapimwa hayatarudishwa kwa wananchi.
"Maeneo yote ambayo tulikwisha kuyapima hayatarudishwa aidha tunahitaji kuchukua maeneo zaidi na tayari nimemuelekeza Mchumi kuandika andiko la kuomba mkopo ili tuweze kuchukua maeneo zaidi, na halmashauri itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia na kuzidi kibuni vyanzo vya fedha ili kuweza kulipa deni lote la fidia”. Ndugu Kibamba alifafanua
Hata hivyo Wakili Kibamba alisema kuwa hadi sasa Halmashauri imefanikiwa kulipa fidia kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya mradi wa upimaji eneo la Nyafula, barabara za Buswelu – Nyamadoke chini ya mradi wa TACTIC, pamoja na taasisi za umma kama vile shule za msingi na sekondari.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.