Baraza la biashara Ilemela limefanyika likiwa na lengo la kuhakikisha yanawekwa mazingira bora kwa wafanyabiashara ili mwisho wa siku waweze kulipa kodi kwa serikali kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Kwa nyakati tofauti wajumbe walipongeza Ilemela kwa namna ambavyo wamekuwa wepesi kuzitatua changamoto zinazowasilishwa huku wakiomba utatuzi kwenye masuala ya ushuru wa huduma, ukosefu wa boti za doria, ukosefu wa maji viwandani, ushuru wa taka katika masoko ya mbao na mengineyo.
Nae Ndugu Gabriel Kenene ambae ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo akitokea chemba ya biashara Mkoa ametumia kikao hicho kuipongeza serikali kwa namna ambavyo imeendelea kutatua changamoto mbalimbali za watanzania akitolea mfano uboreshaji wa miundombinu sekta ya afya na elimu, ujenzi wa daraja la busisi na mengine mengi ambayo serikali inaendelea kuyatekeleza.
Sambamba na pongezi hizo Ndugu Gabriel amehimiza suala la ushirikishwaji katika masuala mbalimbali pamoja na kuomba tozo zinazoumiza wananchi ziangaliwe, uwekaji wa taa za barabarani pamoja na kuhakikisha suala la usafi linakuwa agenda ya kudumu ili kuwepo na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara huku akiwataka wamachinga kuepusha vurugu na kupunguza malalamiko yasiyo na tija ili Ilemela itengeneze Mwanza mpya.
"Lengo kuu la serikali ni kumhudumia mwananchi apate huduma bora kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ili kodi iweze kulipwa hivyo tuna kila sababu ya kuipongeza serikali kwa hatua mbalimbali zinazoendelea",alisema Ndugu Gabriel
Akihitimisha kikao hicho Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela Ndugu Said Kitinga ambae ndio alikuwa Mwenyekiti amehimiza suala la ushirikiano kwani wote sekta za umma na binafsi zinajenga nyumba moja na kuahidi kuwa changamoto zote zilizowasilishwa zitatafutiwa ufumbuzi.
Baraza la biashara Ilemela hujumuisha serikali na wadau kutoka sekta binafsi wakiwemo viongozi wa makundi mbalimbali ya biashara, wawakilishi wa wafanyabiashara, chemba ya biashara mkoa,taasisi za serikali pamoja na wadau wa maendeleo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.