Baraza la madiwani wa Manispaa ya Ilemela limeijadili na kuipitisha rasimu ya mpango na bajeti ya mwaka 2024/2025 ya kiasi cha shilingi Bilioni 81.45 kwa ajili ya matumizi ya Manispaa ya Ilemela ambayo itajumuisha ,mishahara ya watumishi ,ruzuku ya miradi ya maendeleo, ruzuku ya matumizi ya kawaida, miradi ya maendeleo na mapato ya ndani.
Wakiijadili bajeti hiyo katika nyakati tofauti waheshimiwa madiwani wamepongeza kwa namna ambavyo bajeti hiyo inaenda kugusa sekta mbalimbali, huku wakihimiza kuwa isiwe bajeti ya kuishia kwenye makaratasi bali iwe ni bajeti inayotekelezeka.
Sambamba na hilo, Madiwani hao wametilia mkazo suala la ukamilishaji wa miradi viporo hususan ambayo ilianzishwa na wananchi ili kuweza kuunga juhudi za wananchi na kuwatia moyo kuendelea kushiriki katika uanzishaji wa miradi mipya na shughuli za maendeleo kwa ujumla
Akiwasilisha rasimu ya mpango na bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Ndugu Herbert Bilia ambae ni Mchumi wa Manispaa alibainisha kuwa kupitia chanzo cha mapato ya ndani halmashauri inayo mpango wa kuanzisha shule za Sekondari mbili za mfano katika kata za Buswelu na Ilemela sambamba na maboresho ya miundo mbinu mbalimbali katika sekta ya zote.
“Katika vipaumbele vilivyoletwa kutoka katika kata kupitia WDC mahitaji makubwa ni sekta za afya, elimu sekondari na msingi, kwa kuliona hilo, kupitia mapato ya ndani katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa upande wa elimu tunatarajia kujenga shule mbili za sekondari za mfano katika kata za Ilemela eneo la Lumala na Kata ya Buswelu kufuatia kwamba maeneo hayo yamezidiwa na idadi kubwa ya wanafunzi”, Alisema Ndugu Bilia.
Kwa upande wa sekta ya Afya Ndugu Bilia aliendelea kufafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia mapato ya ndani Halmashauri inatarajia kujenga kituo cha afya katika kata ya Ibungilo ili kupunguza msongamano katika kituo cha afya Buzuruga.
Aidha alisema kuwa Halmashauri inatarajia kutumia fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya sekta ya miundombinu ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 1.1 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara katika kata zote 19 za Manispaa ya Ilemela, ambapo Halmashauri kupitia mapato ya ndani inaendelea na mchakato wa manunuzi ya mitambo ya kisasa kwa ajili ya matengenezo ya barabara.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe.Renatus Mulunga amehitimisha kwa kuhimiza juu ya suala la utekelezaji wa bajeti hiyo na kuwataka watendaji kwenda kuisimamia ipasavyo kwa ajili ya maendeleo ya Ilemela huku akihimiza juu ya suala la ushirikiano
“ Kupitisha bajeti ni suala moja, na utekelezaji wa bajeti ni suala jingine twendeni tukaisimamie iweze kutekelezeka” alihitimisha
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.