Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali- Ilemela
Halmashauri ya manispaa ya Ilemela inatarajia kuanza utekelezaji wa zoezi la uchanjaji wa mifugo tarehe 03 Julai 2025 zoezi ambalo litadumu kwa muda wa takriban wiki mbili ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kupunguza na kutokomeza vifo vya mifugo vitokanavyo na magonjwa ya homa ya mapafu ya ng'ombe, sotoka ya mbuzi, kideri kwa kuku, ndui na mafua makali ya kuku.
Katika manispaa ya Ilemela zoezi hili la uchanjaji litatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itahusisha uchanjaji wa kuku wa asili wanaokadiriwa kufikia elfu sabini huku awamu ya pili itahusisha uchanjaji wa ng'ombe na mbuzi sambamba na uwekaji wa hereni kwa ajili ya utambuzi na itaanza mara baada ya kupokea vifaa vingine kama friji, pikipiki sindano vishkwambi n.k
Akikabidhi chanjo hizo kwa maafisa mifugo leo tarehe 02 Julai,2025, Ndugu Petro Joseph ambae alimwakilisha kaimu mkurugenzi amesema kuwa manispaa ya Ilemela imekwishapokea chanjo elfu 23 za ng'ombe, chanjo elfu 70 za kuku na chanjo elfu 28 za mbuzi pamoja na baadhi ya vitendea kazi.
"Niwatake kuhakikisha kuku wote wanaofugwa ndani ya manispaa ya Ilemela wanachanjwa, sambamba na kutoa elimu kwa wafugaji ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria na taratibu wakati wa utekelezaji wa zoezi hili", amesisitiza Ndugu Peter
Naye Dkt. Nelson Rugaimukamu, afisa mifugo wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa chanjo hizi bure na kutoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu wakati wa zoezi hili kwani itawasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa mifugo yao na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa yanayosababishwa na kukosekana kwa chanjo
Akizungumza kwa niaba ya maafisa mifugo wa halmashauri Ndg. David Wanoka, afisa mifugo kata ya Kayenze amesema kuwa amezipokea chanjo hizo na ameahidi kuwa watahakikisha zoezi la utoaji wa chanjo hizo linafanyika kwa ufanisi katika kata zote.
Kampeni hii ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo ilizinduliwa rasmi na Rais Mhe Samia Suluhu Hassan Juni 16,2025 mkoani Simiyu itatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2025/2026.
MWISHO
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.