Na Paschalia George na Yusuf ludimo, Ilemela
Rushwa ni adui wa maendeleo ,hivyo ni jukumu la jamii nzima kutambua ubaya wa rushwa ili iwe rahisi kuepukana nayo. “Anaetoa au kupokea rushwa wote wanafanya makosa” amesema Ndugu Said Kitinga
Ndugu Said Kitinga, ambae ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela ameyasema hayo alipomwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela katika zoezi la kuzindua muongozo wa mafunzo wa kupambana na rushwa ambayo yatahusisha wataalam wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Chama cha Skauti Tanzania ndani ya wilaya ya Ilemela.
Aliongeza kusema kuwa mambo yamekuwa hayaendi yanavyopaswa kwenda kwani jamii ikishajiaminisha kwenye uwepo wa kitu kidogo ndo chachu ya jambo fulani kufanyika kwa haraka na kwa ufanisi lazima jamii husika isue sue katika masuala ya kimaendeleo.
‘’ Rushwa ni adui wa haki,ni muhimu kwa jamii yetu kuwalea watoto kwa kuwapatia elimu hii juu ya madhara ya rushwa toka wakiwa wadogo wakue wakichukia na kupinga rushwa.Viongozi wenzangu bado tunao wajibu mkubwa wa kufikisha elimu kwa jamii nzima,naomba jambo hili likahusishe kila mmoja kwa nafasi yake na tukemee kuhusu adui huyu mkubwa wa maendeleo”amesema Kitinga .
Nae Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Ilemela Norbert Ndika amefafanua kuwa uzinduzi wa muongozo huu kwa kushirikiana na jeshi la skauti Tanzania ni mpango wa serikali wa kuendelea kusambaza elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa kutumia vijana wa skauti ambao tayari wamepitia mafunzo ya awali ya uzalendo na wanauwezo wa kuhamisha elimu hii katika makundi tofauti tofauti ndani ya jamii wanazoishi kama vile shuleni na mpaka ngazi ya kaya.
“Tunatarajia shule zetu zote ndani ya Ilemela kuwa na vikundi vya mapambano dhidi ya rushwa ndani ya shule ambapo vijana hawa watapewa mafunzo ya kupambana na rushwa elimu ambayo wao watapaswa kuifikisha kwa wenzao ndani na nje ya shule.Tunataka jamii itakayohoji matumizi mabovu ya fedha pale inapoonekana sio sahihi sambamba na kuibua makosa au vitendo viovu vinavyochochea au rushwa yenyewe.”amesema kamanda Ndika.
Rushwa imekuwa adui katika maeneo mengi hasahasa maeneo ya kutolea huduma za umma kama vile elimu ,afya na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Uwepo wa rushwa maeneo hayo unazolotesha huduma hizo na kusababisha watumishi au wahusika kutokufanya kazi kwa weledi wao na hivyo kusubiri mpaka wapate kitu flani cha kuwanufaisha ndipo huduma itolewe.
Kamishna wa skauti wilaya ya Ilemela Jesca Ndelwa ameupokea mpango huu kwa furaha kubwa huku akiahidi ushirikiano wa kiwango cha juu kabisa katika kutoa elimu hiyo umma.
“Hatutokaa kimya kuruhusu rushwa iendelee kututawala,tutatoa elimu ya kutosha kwa vijana wetu wa skauti na wao wataitoa kwa wengine, tutaendelea kusambaza elimu hiyo kwa namna mbalimbali zenye tija kwa jamii yetu ya Ilemela”amesema Kamisha Ndelwa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.