Jumuiya ya mamlaka ya serikali za mitaa (ALAT) mkoa wa Mwanza imeipongeza manispaa ya Ilemela kwa kutenga fedha na kuanza ujenzi wa barabara ya hospitali ya Wilaya kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.3.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya manispaa ya Ilemela Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Mwanza ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Magu Mhe. Mpandalume Simon amesema kuwa manispaa ya Ilemela inastahili pongezi kwa uthubutu wa kutenga fedha za mapato ya ndani na kuanza ujenzi wa barabara hiyo licha ya jukumu la usimamizi na ujenzi wake kuachiwa wakala wa barabara za mijini na vijiji (TARURA).
" ALAT mkoa wa Mwanza tunaipongeza Ilemela chini ya Mwenyekiti wake, Mkurugenzi na wataalam wote kwa kutenga fedha zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii, Bilioni moja kwa awamu ya kwanza na nyingine itatumika awamu ya pili kukamilisha mradi huu , sisi wa kutoka halmashauri nyingine tunalo la kujifunza ." Alisema
Aidha Mhe. Mpandalume amemshauri Meya wa manispaa ya Ilemela kuhakikisha anasimamia vizuri malipo ya mkandarasi anaetekeleza mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo , Mhandisi Jacob Buswege kutoka TARURA wilaya ya Ilemela amesema kuwa mradi unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi millioni 904.47 hadi kukamilika kwake na kuongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza Juni 12, 2023 kupitia mkandarasi Kaserkandis Construction & Transport Co. Ltd ya mkoani Mwanza.
Nae mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela Mhe. Renatus Mulunga amesema kuwa kufanikiwa kwa miradi inayotekelezwa ndani ya manispaa yake ni kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kwa uongozi mzima kuanzia Mbunge wa Jimbo hilo Dkt. Angeline Mabula, Mkuu wa wilaya Mhe. Hassan Masala, Baraza la madiwani ,mkurugenzi na viongozi wa CCM.
Wajumbe wa ALAT mkoa wa Mwanza wapo wilaya ya Ilemela kwa wa ziara ya siku mbili ambapo miradi mingine iliyotembelewa ni ujenzi wodi katika hospitali ya Wilaya ya Ilemela Sangabuye na ujenzi wa shule mpya ya msingi Butuja iliyopo kata ya Kahama.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.