Jumla ya watoto 819 ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika mitaa mbalimbali wamepata huduma mbalimbali za afya ikiwemo lishe bora ,chanjo,matibabu ya watoto sambamba na mapishi kwa vitendo kupitia jiko darasa.
"…tulikusudia kuhudumia watoto 700 mpaka mwisho wa zoezi kwa awamu ya kwanza tumehudumia watoto 819 sawa na asilimia 117.Huduma hizi ni mwendelezo kwa kila robo ya mwaka.." Amesema afisa lishe wa Manispaa hiyo Bi. Pili Khasim wakati wa maadhimisho hayo katika mtaa wa Isesa kata ya Sangabuye.
Bi.Pili ameongeza kuwa jumla ya watoto 172 kati ya 819 sawa na asilimia 21 ya watoto wote waliohudumiwa wamegundulika kuwa na udumavu na kuanzishiwa matibabu, elimu ya lishe bora imetolewa kwa wazazi wao huku wahudumu wa afya ngazi za mitaa wakiendelea kuwa karibu na familia zenye changamoto hizo kwa ajili ya ushauri pale inapobidi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imedhamiria kuendelea na maadhimisho hayo kwa kutoa huduma za kiafya kama vile vipimo vya urefu na uzito ,chanjo mbalimbali, vidonge vya minyoo, matone ya vitamin A na tathimini ya hali ya lishe lengo ikiwa ni kupunguza na kutokomeza kabisa changamoto za udumavu na utapiamlo.
Leah Mabula ni mkazi wa mtaa wa Isesa anapongeza timu nzima iliyofika kutoa huduma za afya mtaani kwao kwa usikivu wao na weledi waliouonyesha kwa watu wote waliohudumiwa.
Maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya mtaa kwa awamu ya kwanza yamefanyika kwenye kata za Kayenze,Sangabuye na Bugogwa katika mitaa 10 ya Lutungo, Iseni, Igalagala, Nyafula, Isesa, Imalangombe, Kabangaja, Igombe B, Sangabuye na Bezi ambapo zoezi hilo limefanyika kwa kushirikiana shirika la USAID kupitia mradi wake wa afya yangu mama na mtoto.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.