Ikiwa imesalia takriban miezi mitano kufika ukomo wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) walengwa wa mpango huo wameaswa kuendelea na utaratibu wa kuwekeza kwenye vikundi walivyovianzisha wao wenyewe vya kuweka akiba na kukopeshana ikiwa ni njia ya kukuza mzunguko wa fedha sambamba na kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha walizozipata kupitia mfuko huo.
Akizungukumza na walengwa wa kata ya Buswelu wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha kwa kipindi cha Januari – Februari ,2025 mwezeshaji kutoka TASAF Ilemela Eva William amesema ni muhimu kwa walengwa wote kuendeleza utamaduni wa kujishughulisha na shughuli ndogo ndogo za kuwaingizia kipato na kuweka akiba.
“.. Mpango huu unaelekea kufika mwisho,wengi hapa mmenufaika kwa namna tofauti tofauti kuna watu walikuwa wanakula mlo mmoja sasa hivi wanakula milo miwili hadi mitatu,muendelee kuwekeza kwenye vikundi vyenu vya kukopeshana ili kutoruhusu hali ya umaskini mliyokuwa nayo awali irudi tena . .”
Nae mratibu wa TASAF Manispaa ya Ilemela Leonard Robert ametoa rai kwa walengwa hao kuhusu ukomo wa mpango wa kunusuru kaya za walengwa (PSSN II) ifikapo Septemba 2025 huku akiwasihi walengwa kujipanga kisaikolojia na kuendeleza vikundi vyao kwa ajili ya kujiandaa kujitegemea na kujiimarisha zaidi kiuchumi.
Hellena Ndutwa ni mkazi wa mtaa wa Bulola A uliopo kata ya Buswelu yeye anakiri kunufaika na TASAF kwa kipindi cha miaka mitano akiwa mlengwa kwa kufanikiwa kusomesha jumla ya watoto 5 ambapo watatu wapo sekondari na wawili shule ya msingi na mmoja anaendelea kupatiwa huduma za afya kliniki.
“..ninafuraha hata kama mpango unakwisha lakini nina nafuu ya maisha watoto na wajukuu zangu wameshavuka hatua flani kielimu na mimi sijakaa tu najishughulisha na kilimo cha mboga mboga na ninafanya vibarua vya kulima na shughuli mbalimbali za majumbani zinazoniingizia kipato,kwa kweli TASAF wamenitoa gizani.."
Jumla ya kiasi cha shilingi milioni 131,381,298.00 zinatarajiwa kutolewa kwa kaya maskini 3,545 ambapo kaya 29 zitalipwa pesa taslimu na kaya 3,516 zinalipwa kwa njia ya mtandao (kupitia simu na benki) ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikihusisha mitaa yote 171 katika zoezi la malipo ya mkupuo mmoja wa dirisha la Januari/Februari ,2025 lililoanza leo tarehe 28 hadi 30 Aprili, 2025.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.