Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi.Ummy Wayayu amesisitiza utolewaji wa huduma bora za afya kwa wateja wote wanaopatiwa huduma hizo ndani ya vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo ndani ya Manispaa hiyo ikiwa ni sehemu ya watumishi wa idara ya afya kuwajibika ipasavyo kwa lengo la kutoa huduma za viwango vinavyokubalika.
Akizungumza na timu ya wataalam wa kusimamia huduma za afya katika vituo vya afya vilivyopo ndani ya Manispaa hiyo wakati wa kikao cha kawaida kujadili mwenendo wa takwimu na utendaji kazi kwa kipindi cha Julai – Desemba 2024/2025 Bi.Ummy amewataka wataalam hao kuendelea kutoa huduma nzuri kwa watu wote kwa kuzingatia umuhimu mkubwa wa suala la afya .
“..afya ni jambo nyeti sana,bila kuwa na afya nzuri huwezi kufanya kitu chochote ninyi mna jukumu la kuhakikisha jamii inakuwa salama nataka wananchi wetu wote wahudumiwe kwa usawa wanapokwama waelekezwe..”
Ameongeza kuwa ni lazima kwa vituo vyote kutoa huduma kupitia mifumo ya afya ya kieletroniki iliyowekwa na serikali huku akiahidi kutatua changamoto ya mtandao katika baadhi ya maeneo ndani ya Manispaa yake.
Akitoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo mganga mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dkt.Maria Kapinga amesema timu yake ya wataalam wa afya wanaendelea kufanya kazi kubwa ya kuelekezana wao kwa wao kupitia vikao kama hivyo ili kuleta maboresho kila siku na kupongeza wataalam wa chanjo kwa kufikia malengo huku zoezi la elimu kwa umma likiendelea nyumba kwa nyumba.
Mkurugenzi Ummy ametoa pongezi kwa kazi nzuri inayofanywa na idara ya afya Ilemela ya kutoa taarifa zake za fedha kwa weledi na kwa wakati hali inayoisaidia taasisi yake kuona mapungufu mapema na kuyatafutia ufumbuzi huku akizitaka idara zingine za Manispaa hiyo kuiga mfano huo.
Aidha Bi.Ummy ametoa vyeti vya pongezi kwa vituo vya afya vilivyofanya vizuri katika matumizi ya mfuko wa pamoja wa huduma za afya (HSBF) ambao ni kituo cha afya Karume na zahanati ya Kirumba huku walioongoza kwa huduma ya chanjo wakiwa ni kituo cha afya Buzuruga na zahanati ya Kabusungu na vituo vilivyoongoza kwa ukusanyaji wa mapato Buzuruga kituo cha afya na zahanati ya Pasiansi.
“..Inatia moyo kuona viongozi wetu wanatambua mchango wetu,tunaahidi kuwa bora zaidi katika utoaji huduma za afya kwa wateja wetu..”amesema mgaganga mfawidhi wa kituo cha afya Buzuruga Dkt.William Ntinginya
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.