Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake kwa kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuleta madhara makubwa duniani kwa sasa.
Hayo yamezungumzwa na mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mwanza kwenye viwanja vya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara yanayoadhimishwa nchini kila tarehe 09 Desemba ya kila mwaka tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mnamo mwaka 1961.
“..Uhuru ni haki ya msingi ya kila mtu au taifa kuamua kufanya mambo bila kuingiliwa na mtu yoyote ki maamuzi…” Amesema Cde.Ngubiagai akimnukuu hayati baba wa taifa la Tanzania Mwl.Julius Kambarage Nyerere
Cde.Ngubiagai ameongeza kuwa pamoja na shughuli mbalimbali ambazo zinafanyika katika maadhimisho hayo ni muhimu kuwaenzi waasisi wa taifa kwa kuzingatia misingi ya uhuru ambayo inajumuisha umoja,usawa,uwajibikaji,kujitegemea na haki za binadamu ili kuleta maendeleo kwa kasi.
“..Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoendelea nayo ya kuleta maendeleo,kipindi cha uhuru mkoa wa Mwanza ulikuwa na shule 5 tu leo tuna jumla ya shule 332 na nyingine zinaendelea kujengwa..”
Aidha Afisa usalama mstaafu wa mkoa wa Mwanza Dkt.Jason Mutashi ametoa mada kuhusu amani wakati wa kongamano lililojikita zaidi katika masuala ya uhuru wa Tanzania bara, amesema nchi hiyo ilipata uhuru wake kwa njia ya amani bila kumwaga damu na kwamba nchi iliongozwa kwa kufuata misingi ya amani ,umoja na uadilifu bila kujali dini wala makabila ya mwananchi wake.
“.. Hatuna budi kuilinda tunu ya taifa letu ambayo ni amani..” amesema Dkt.Mutashi
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mstaafu Dkt.Leonard Masale amesema Tanzania bara inatimiza miaka 62 ya jamhuri huku akifafanua maana jamhuri kuwa ni jamii huru
“..Nyakati za nyuma hali ya maendeleo haikuwa nzuri,sekta ya elimu ,afya miundo mbinu ya barabara ilikuwa duni sana ndo kisa cha hayati baba wa taifa Mwl.Nyerere kuanzisha vita dhidi ya maadui watatu ambao ni maradhi ,umaskini na ujinga ,vita ilozaa matunda chanya tunayoyaona leo..”
Hoja Misong’hwani ni mwenyekiti wa mtaa wa Kadinda katika kata ya Kahama ndani ya Manispaa ya Ilemela yeye anasema kumekuwa na maendeleo mengi makubwa mtaani kwake akilinganisha na hali ilivyokuwa wakati wa uhuru huku akikiri kuwepo kwa huduma za maji na umeme kwenye mtaa wake vitu ambavyo havikuwepo awali.
Maadhimisho hayo yamepambwa na kauli mbiu isemayo uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa wananchi ni msingi wa maendeleo yetu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.