Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala ameridhishwa na kupongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa shule ya sekondari kata ya Buzuruga itakayogharimu kiasi cha shilingi milioni mia nne na sabini mpaka kukamilika kwake.
Mhe Masala amebainisha hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ndani ya wilaya hiyo akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, wataalam wa manispaa ya Ilemela na baadhi ya viongozi wa Chama tawala (CCM). Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya wilaya utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni mia nane, ujenzi wa kituo cha afya Kayenze wenye kiasi cha shilingi milioni mia tano, na ujenzi wa shule mpya ya sekondari Buzuruga ambapo amewataka wananchi, wataalam na viongozi wa maeneo inapotekelezwa miradi hiyo kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ikizingatia ubora unaotakiwa kwa gharama nafuu zilizopangwa.
‘.. Tumetembelea miradi ya maendeleo kukagua nini kinaendelea, na tutaendelea kufanya hivyo kadri tunapopata nafasi, Naridhishwa na kasi ya ujenzi wa hapa Buzuruga kikubwa tuzidi kujitahidi ili mradi huu ukamilike kwa wakati ..’ Alisema
Aidha Mhe Hasan Masala amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo huku akiwaasa mafundi waliokabidhiwa jukumu la ujenzi kuhakikisha hakuna ubadhirifu wowote utakaojitokeza na wajumbe wa kamati za ujenzi kuwa makini katika usimamizi wa vifaa vya ujenzi kwa kuwa Serikali haitavumilia ubadhirifu wowote utakaojitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Joseph Apolinary amewahakikishia wananchi kuwa fedha ya utekelezaji wa miradi hiyo ipo kikubwa ni mafundi kuongeza kasi ya ujenzi ili kwenda sambamba na kalenda ya bajeti ya Serikali kuepuka kurudishwa kwa fedha hizo Serikali kuu.
Crydon Gondwe ni miongoni mwa wajumbe wa kamati wanaosimamia ujenzi wa shule ya sekondari Buzuruga ambapo ameshukuru viongozi hao kutemebelea mradi huku akiahidi ushirikiano kwa niaba ya wananchi wengine.
Kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Ilemela itaendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya wilaya hiyo wiki ijayo kwa kutembelea miradi ya barabara na mengineyo kadri ya itakavyopangwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.