Baraza la Madiwani Ilemela limekutana na TARURA Wilaya ya Ilemela kwa ajili ya kujadili ajenda moja ya mustakabali wa barabara zinazopatikana katika Manispaa ya Ilemela
Wakiwasilisha hoja zao juu ya barabara zinazopatikana katika kata zao waheshimiwa madiwani katika nyakati tofauti, mbali na kuipongeza TARURA kwa jitihada zake wameitaka kuhakikisha kuwa barabara zote za Manispaa ya Ilemela zinawekwa katika mpango wa matengenezo na zinatengenezwa kwa viwango cha mawe au zege ili ziweze kudumu.
Pamoja na hilo wameitaka TARURA kuhakikisha kuwa wanatengeneza mitaro na makalavati imara ili kuwezesha barabara hizo kudumu na zisiharibiwe na mvua zinazoendelea huku wakiwataka kukamilisha barabara hizo kwa wakati na ili zipitike katika nyakati zote.
Aidha wameitaka TARURA kuhakikisha barabara ambazo zinaelekea katika taasisi mbalimbali kama shule hospitali na zingine kuhakikisha zinapewa kipaumbele kwani ndipo sehemu wananchi huenda kupata huduma za kijamii.
Mhandisi Sobe Makonyo kutoka TARURA akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa matengenezo ya barabara Wilaya ya Ilemela amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya mikataba 9 ya utengenezaji wa barabara inatarajiwa kutekelezwa na hadi sasa mikataba 7 imeshaingiwa kati ya miradi hiyo saba miradi miwili imekamilika, miradi 5 inaendelea na miradi miwili ipo hatua ya manunuzi.
Ameongeza kusema kuwa TARURA Wilaya ya Ilemela imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 2.6 katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ambapo Shilingi Bilioni 1.6 ni kutoka bodi ya barabara, Milioni 500 ni fedha za mfuko wa Jimbo na Shilingi Bilioni moja ni fedha za tozo za mafuta na kuongeza kuwa hadi sasa fedha iliyoidhinishwa ni kiasi cha Shilingi Milioni 500 .
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa Ilemela imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2 itakayotoka katika mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya matengenezo ya barabara ikiwa ni maelekezo ya Serikali kuu ya kuzitaka halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya barabara.
Mhe Renatus Mulunga, Mstahiki Meya wa Ilemela ameishauri TARURA kutengeneza barabara za mawe na mitaro imara kutokana na kuwa kata nyingi zipo kwenye mwinuko ili ziweze kudumu na thamani ya fedha ionekane.huku akihimiza usimamizi mzuri na juhudi katika matengenezo ya barabara hizo.
“Niwatake TARURA kuanza kufikiria kutengeneza barabara za mawe ili ziweze kudumu muda mrefu kwani kata nyingi za Manispaa ya Ilemela zipo kwenye mwinuko”amesema Mhe Mulunga
Pamoja na hayo Mstahiki Meya, amemtaka Mkurugenzi na wataalam wote kuhakikisha wanatilia mkazo suala la ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha upatikanaji wa shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na kusisitiza kuwa fedha hiyo itatolewa katika kata zote kwa uwiano sawa ambapo amewataka Madiwani kuainisha barabara chache ili zitengenezwe katika ubora na thamani ya fedha iweze kuonekana.
“Tumepitisha kwa kauli moja kuwa kupitia fedha hizo za mapato ya ndani kila kata itapata fedha kiasi cha Shilingi milioni 63 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na hivyo niwashauri madiwani watengeneze barabara chache ili thamani ya fedha iweze kuonekana”, Amesisitiza Mhe Mulunga
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inao mtandao wa barabara wa Km 875.75 Barabara za lami ni Km 35.26, zege Km 1.52, mawe Km 2.07, Changarawe km 60.18, Udongo km 776.83
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri Ya Manispaa ya Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.