Madiwani wa Ilemela wametakiwa kuwajibika na kuwa wawazi, hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela John Wanga, katika semina elekezi iliyotolewa kwa madiwani hao ambao walikula kiapo siku ya tarehe 02/12/2020.
Semina hiyo elekezi iliyofanyika kwa muda wa siku tatu ililenga kuwajengea uwezo waheshimiwa madiwani hao ili waweze kutekeleza majukumu mbalimbali katika kuhakikisha wanaleta maendeleo yenye tija katika kata zao na halmashauri kwa ujumla.
Aidha aliwataka pamoja na kujenga mazingira bora katika kuwawezesha wananchi ili waweze kutekeleza miradi ya maendeleo pia aliwataka kujitahidi kutokuanzisha na kupunguza migogoro isiyokuwa na tija.
Katika semina hiyo ambayo pia iliwahusisha wataalam wa Manispaa ya Ilemela ambao ndio walikuwa watoa mada wakuu, madiwani waliweza kujua mfumo wa serikali za mitaa misingi yake, namna inavyoendeshwa na sharia mbalimbali zinazotawala muundo na nidhamu ya serikali za mitaa. Halikadhalika waliweza kuelekezwa masuala mbalimbali kuhusiana na dhana nzima ya utawala bora pamoja na kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Afisa Usalama wa Wilaya nae aliwasilisha mada kuhusiana na utunzaji wa siri za vikao na kuwaelekeza kuwa madiwani ndio wanaosimamia mustakabali wa halmashauri.Pia aliwataka waweze kuchunga mienendo yao kwani mienendo huakisi tabia na maisha kwa ujumla ili waweze kuwatumikia wananchi ili kuweza kufikia maendeleo tarajiwa.
Mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo mahusiano ya kisheria kati ya serikali kuu na serikali za mitaa,pamoja na sharia mbalimbali ambazo zitawaongoza katika kutekeleza majukumu kama viongozi wa wananchi ikiwa ni pamoja na sharia ya maadili ya viongozi wa umma, sharia ya serikali za mitaa.
Aidha walitakiwa kuwa na mahusiano mazuri na watendaji mbalimbali kuanzia ngazi ya Halmashauri hadi ngazi ya mtaa ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi waliwachagua.Pamoja na hayo walikumbushwa kuepukana na rushwa mbalimbali.
Nao madiwani walishumkuru Mkurugenzi wa Manispaa kwa kupatiwa semina hiyo elekezi ambapo wameweza kujifunza masuala mbalimbali na kuomba ushirikiano kutoka kwa wataalam pamoja na kuahidi kuwa watatekeleza majukumu yao na kuzingatia kiapo cha uadilifu walichoapa ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wa Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.